CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kimetoa mafunzo maalum kwa Waandishi wa Habari yenye lengo la kujua kwa kina uhifadhi, uwindaji na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yaliyofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), yanafanyika Bagamoyo mkoani Pwani, yakihusisha waandishi wa Habari 30, kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuwajengea uwezo wanahabari katika  kusimamia na kuandika habari za Uhifadhi, uwindaji haramu na usafirishaji wa wanyamapori.

Akizungumza na RAI juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, alisema kuwa chama hicho kimedhamiria kujikita katika kupaza sauti juu ya masuala ya uhifadhi, uwindaji na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Alisema ili kufanikisha hilo wameiona haja ya kushirikiana na USAID PROTECT kuwajengea uwezo waandishi wa habari katika mikoa mbalimbali nchini.

Chikomo alisema kiu ya JET kwa sasa ni kuona Tanzania inakuwa kimbilio kubwa la watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani na ili kufanikisha hilo ni lazima kuwa na utanzaji wa mazingira na wanyamapori.

“Jukumu letu ni kupaza sauti ya juu ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kupaza sauti yetu kwenye maeneo mbalimbali, lakini tumeona haitoshi ni vema kama tutatanua wigo kwa kuangalia ni namna gani tutakuwa na sauti ya pamoja katika kukemea uwindaji, usafirishaji haramu na hifadhi za wanyama,”alisema Chikomo.

HISTORIA YA UHIFADHI NCHINI

Uhifadhi una historia ndefu duniani, hata hivyo kwa Tanzania historia ya uhifadhi wanyapori inaanzia mwaka 1891 wakati sheria za kudhibiti uwindaji zilipoanzishwa na utawala wa Wajerumani.

Sheria hizi zilidhibiti uvunaji wa wanyama, mbinu za uwindaji na biashara ya wanyamapori.

Ikumbukwe kuwa wanyamapori  ni urithi wa asili wa pekee na rasilimali yenye  umuhimu mkubwa kimataifa.

Umuhimu wake umejikita katikathamani ya kibiolojia ya aina za wanyama na mazingira ya asili yaliyopo duniani.

Mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori ndiyo msingi wa tasnia ya matumizi endelevu ya wanyamapori.

Matumizi endelevu ya wanyamapori ni pamoja na kutazama wanyama, uwindaji wa kitalii, uwindaji wa wakazi na ufugaji wa wanyamapori.

Pamoja na hayo yote, bado eneo hili ambalo lina nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa taifa haijaweza kuendelezwa kufikia malengo kutokana na kutokuwepo na Sera ya Wanyamapori iliyo wazi.

Aidha kutokuwepo na mwamko juu ya uhifadhi wa wanyamapori miongoni mwa wapangaji mipango na maafisa wenye mamlaka huchangia suala hili kupewa uzito mdogo.

Ongezeko la idadi ya watu na shughuli mbalimbali huchangia kutoweka kwa makazi ya wanyamapori.

Miongoni mwa maeneo yanayoathiri uhifadhi ni kuongezeka kwa ujangili na biashara isiyo halali ya wanyamapori.

Kukosekana kwa imani kati ya Serikali na wananchi waishio pembezoni  mwa hifadhi kunachangia kushamiri kwa uwindaji haramu.