Biashara haramu ya mbao Kilwa sasa moto wa nyika

WAKATI vijiji vya wilaya ya Kilwa vimeanza kunufaika na mpango wa Serikali wa Menejimenti Shirikishi ya Misitu (Participatory Forests Management - PFM) uliowezesha kutengewa misitu kadhaa ya hifadhi, limeibuka tatizo jipya – kukithiri kwa biashara haramu ya mbao na magogo wilayani humo.
 
Maofisa kadhaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa waliuambia ujumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) uliotembelea wilaya hiyo, hivi karibuni, kwamba mbao na magogo yanayotokana na uvunaji haramu katika misitu ya wilaya hiyo hupelekwa Comoro kupitia Zanzibar.
 
Viongozi wa vijiji kadhaa vilivyotengewa na Serikali misitu ya hifadhi ambavyo ujumbe huo wa JET ulivitembelea walieleza, hata hivyo, kwamba tatizo hilo lipo katika misitu iliyo chini ya usimamizi wa Serikali Kuu au ile ya Halmashauri na si katika misitu iliyotengwa kwa vijiji hivyo.
 
“Sisi doria zetu ni kali. Si rahisi mtu yeyote akiwamo mwanakijiji kuingia katika misitu yetu na kukata mbao bila kibali. Ni dhahiri tatizo hilo lipo zaidi kwenye misitu iliyo chini ya usimamizi wa Serikali au ile iliyo chini ya Halmashauri na si hii tuliyotengewa na tunayoisimamia sisi,” anasema Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Nainokwe, Yassin Abdallah.
 
Kijiji hicho kipo Kilomita 93 kutoka Kilwa mjini. Akikiri kuwapo kwa tatizo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Adoh Mapunda anasema kuwa wilaya inajitahidi kupambana na tatizo hilo licha ya ukubwa wa wilaya yenyewe.
 
“Kilwa ni wilaya kubwa. Ina Kilomita za mraba 13,000. Ina misitu mingi, na pia ina ukanda mrefu wa pwani wenye bandari bubu nyingi, na hivyo ni kazi ngumu kuidhibiti kwa ukamilifu.
 
“Tunatumia mbinu nyingi kupambana na tatizo hili, lakini njia kubwa tunayotumia ni doria. Tumeimarisha doria zetu. Hivi karibuni tulitumia Sh milioni saba kufanya doria na kufanikiwa kukamata mbao zilizokuwa zisafirishwe nje kinyume cha taratibu, na zilipopigwa mnada tulifanikiwa kupata Sh milioni nane,” anasema Mapunda.
 
Anaeleza kwamba mbao nyingine zilizokamatwa wakati wa doria hizo ziligawiwa kwa shule moja ya sekondari wilayani humo kwa ajili ya kutengeneza vitanda 90 vya kulalia wanafunzi, na nyingine zilitolewa kwa chuo cha ufundi ili zitumike kwa mafunzo ya vitendo (practicals) ya wanafunzi.
 
Akizungumzia suala hilo, Kaimu Ofisa Maliasili wa wilaya hiyo, Abushir Mbwana anakiri kwamba tatizo la uvunaji haramu wa misitu unaostawisha biashara hiyo haramu ya mbao na magogo lipo zaidi kwenye misitu inayomilikiwa na Serikali Kuu, na ile iliyo chini ya Hamashauri kuliko ile inayosimamiwa na vijiji.
 
“Ukweli ni kwamba kila msitu wa Serikali au Halmashauri unastahili kuwa na meneja wake, lakini hilo haliwezekani kwa sababu ya tatizo la rasilimali watu, fedha na vitendea kazi, na hivyo kuna uvunaji mwingi usio halali ndani ya misitu hiyo,” anasema Mbwana. Mbwana anasema kuwa katika hali hiyo, njia ambayo ni lojiki ya kupambana na tatizo hilo kwa sasa ni kuimarisha doria, na pia kudhibiti suala la utoaji vibali vya uvunaji misitu.
 
Kuhusu suala hilo la utoaji vibali vya uvunaji misitu, Mbwana anasema kuwa sasa vibali hutolewa kwa uamuzi shirikishi tofauti na ilivyokuwa zamani kabla Serikali haijaanzisha mpango wa Menejimenti Shirikishi ya Misitu (PFM).
 
“Mwombaji wa kibali ni lazima apitie kwanza kijijini ambako maombi yake hujadiliwa na kukataliwa au kupitishwa katika kikao cha Halmashauri ya kijiji kinachoendeshwa kwa uwazi,” anasema Mbwana. Kwa mujibu wa maelezo yake, maombi hayo yakipitishwa ngazi ya kijiji ndipo yanapoweza kupelekwa ngazi ya wilaya ambako kuna kikao cha Kamati ya Uvunaji Misitu ambacho Mwenyekiti wake ni mkuu wa Wilaya.
 
“Katika kikao hicho cha ngazi ya wilaya, wenyeviti wa vijiji vilivyopitisha maombi hayo ya vibali nao pia hualikwa kuhudhuria. Kikao hupitisha au kukataa maombi kwa kuzingatia mambo mbalimbali kama vile kiasi kinachotakiwa kuvunwa, aina ya miti inayotakiwa kukatwa, na hata rekodi ya mwombaji.”
 
“Kama mwombaji amewahi kushiriki kwenye biashara haramu ya mbao, maombi yake hukataliwa mara moja. Kwa hiyo utaona kwamba uamuzi wa kutoa vibali ni wa pamoja.
 
“Kwa maneno mengine, mchakato wa utoaji vibali kwa wanaoomba kuvuna misitu ni mchakato shirikishi unaoanzia ngazi ya chini kabisa,” anasema Mbwana.
 
Kaimu Ofisa Maliasili huyo wa wilaya anasema pia kwamba ni kwa muktadha huo, misumeno mikubwa (chain saw) ya kukata magogo imepigwa marufuku katika wilaya nzima ya Kilwa.
 
*Akizungumzia mafanikio ya doria zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ambazo zinashirikisha wadau wengine kadhaa, vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama, Mbwana anasema kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja, mbao 1,920 zilikamatwa zikisafirishwa kinyemela nje ya wilaya.
 
“Tuliwakamata pia wahusika kadhaa na kesi ziko mahakamani. Mpaka sasa tumeshashinda kesi mbili ambapo wahusika walitozwa faini,” anasema.
 
Ujumbe huo wa JET ulielezwa katika baadhi ya vijiji uliovitembelea kwamba hata baada ya waombaji kupewa vibali vya kuvuna misitu katika kikao hicho shirikishi cha ngazi ya wilaya, bado huchukua taratibu nyingine kuhakikisha “hawalizwi” na wenye vibali hao.
 
“Kwetu mfanyabiashara hata aje na kibali kutoka ngazi ya wilaya, haturuhusu yeye au wakala wake waingie msituni. Anachotakiwa kufanya ni kutupa kibali chake na sisi ndio tunaotafuta vijana wetu kuingia msituni kumkamilishia mzigo wake kwa mujibu wa kibali chake, na kisha kumkabidhi na sisi kupata ushuru wetu. Tena yeye ndiye hulipia gharama za vijana hao wanaomkatia mbao,” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Kikolle, Mwinyimkuu Hamad Hawadh.
 
Suala la udhibiti wa uvunaji haramu wa misitu unaosababisha kushamiri kwa biashara haramu ya mbao na magogo katika wilaya ya Kilwa linapewa kipaumbele katika vijiji vya wilaya hiyo kiasi kwamba kiwango kikubwa cha mapato ya vijiji yanayotokana na uvunaji misitu huelekezwa kwenye doria.
 
Katika mapato ya kila kijiji yatokanayo na misitu ya hifadhi, ni asilimia tano tu ambazo hupelekwa Halmashauri. Asilimia nyingine 50 hubaki kijijini kwa ajili ya kiuboresha huduma za jamii, na kiasi kingine kilichobakia cha asilimia 45 ndicho huelekezwa kwenye Kamati za Maliasili kwa ajili ya uimarishaji wa doria. Ni fedha hizo zinazoelekezwa kwenye kamati za maliasili zinazotumika kununua pikipiki, baiskeli, ma-ovaroli kwa ajili ya doria, na hata kuwalipa posho kidogo wanaozifanya.
 
Kijiji cha Nanjilinji “A” , kwa mfano, kamati yake ya maliasili imetumia Sh milioni 15 za mapato yake kununua pikipiki kadhaa za doria; jambo linalothibitisha ni kiasi gani kimepania kupambana na biashara haramu ya mbao na magogo katika misitu ambayo kimetengewa na Serikali.
 
Tatizo lililopo, hata hivyo, ni kwamba baadhi ya misitu ya Serikali ambayo inapakana na misitu iliyotengwa kwa ajili ya vijiji ina wanyama, hivyo uwindaji hufanyika kwa vibali vinavyotolewa na Serikali ambavyo mchakato wake haushirikishi vijiji hivyo.
 
Mara nyingine wawindaji hao wakiisha kupewa vibali huingia katika misitu hiyo ya Serikali kuwinda wanyama, lakini wakati mwingine huvuka na kuingia misitu iliyotengwa kwa ajili ya vijiji ama ‘wakifukuzia’ wanyama au kwa lengo la kuvuna mipingo kiharamu.
 
Tatizo hilo lililalamikiwa sana katika mkutano ambao ujumbe huo wa JET ulifanya na Halmashauri ya Kijiji cha Nainokwe. Kila mjumbe aliyesimama kuzungumza alizungumza kwa uchungu kuhusu tatizo hilo. “Wanakuja na vibali vyao vya kuwindia wanyama, wanapiga risasi wanyama, wanawasha moto, na wakati mwingine wanaingia hata katika maeneo ya msitu wetu kufanya mambo hayo.
 
“Wakati mwingine tunaogopa kuwafuatilia maana wana silaha kali na wanapiga risasi ovyo,” alilalamika mjumbe wa Kamati ya Maliasili ya kijiji hicho, Mohamed Twaibu.
 
Twaibu anawalalamikia wawindaji hao kwamba ndio pia wanaosababisha moto katika misitu. “Moto ukishaanza katika msitu wa uwindaji huvuka na kuingia katika msitu wa hifadhi wa kijiji,” analamika mwanakijiji huyo ambaye pia aliwashutumu wawindaji hao kwa kuchafua misitu kwa kutupa ovyo chupa za plastiki za maji na mabaki ya vyakula.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Abdallah Saidi Kigomba, tatizo hilo linaweza kupungua iwapo ungetengenezwa utaratibu wa kushirikisha vijiji wakati wawindaji hao wanaopewa vibali vya kuwinda wanapoingia msituni kuwinda wanyama.
 
“Tunapofanya doria ndani ya misitu yetu tunakuta chupa nyingi za maji za plastiki na hata makopo ya juisi na mabaki ya chakula. Ni dhahiri vitu hivyo vimeingizwa eneo letu la msitu na wawindaji hao. Swali la kujiuliza ni je; wawindaji hao walikuwa wanatafuta nini katika msitu wetu wa akiba? Kwa nini tusiamini kuwa mbali ya kuwinda pia wanakata mipingo”?, aliuliza mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Abdallah Hussein Mpulu.
 
Je, wamewahi kuliwasilisha tatizo hilo kwa mamlaka husika wilayani? “Hatujaliwasilisha rasmi kimaandishi wilayani, lakini tumewahi kulizungumzia katika mikutano yetu ya kawaida na wao, lakini bado hakuna kilichobadilika,” anasema Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Abdallah Saidi Kigomba.
 
Kama ni kweli kwamba baadhi ya wawindaji wanaopewa vibali vya kuwinda wanyama katika misitu ya Serikali ndio hao hao wanaoshiriki biashara haramu ya mbao na magogo; hususan ya Mpingo, basi, tatizo ni kubwa kuliko inavyofikiriwa na uongozi wa wilaya.
 
Vyovyote vile; ikizingatiwa kwamba wilaya ya Kilwa ndio pekee nchini iliyobakia na kiwango kikubwa cha miti aina ya Mpingo, ni vyema uongozi wa wilaya, mkoa na ngazi ya taifa ukashikamana kuikomesha biashara hiyo haramu ya mbao na magogo kabla miti hiyo nayo haijatokomezwa kabisa wilayani humo.
 
Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
mbwambojohnson@ yahoo.com
0718 616199