Misitu yaibua mapya Kilwa

WANAKIJIJI wa Ruhatwe, wilayani Kilwa, wana majuto. Miaka kadhaa iliyopita kijiji chao kilifuatwa na Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo ili kisaidiwe mchakato wa kutengewa na Serikali misitu ya hifadhi inayokizunguka, lakini hawakuichangamkia ‘ofa’ hiyo.
 
Maofisa wa shirika hilo lisilo la kiserikali – Mpingo Conservation and Development Initiative (MCDI) hawakutaka kupoteza muda na kijiji hicho, na hivyo waliviendea vijiji vingine ambavyo viliichangamkia ‘ofa’ hio, na sasa vimetengewa rasmi misitu kadhaa chini ya mpango wa Serikali wa Ulinzi Shirikishi wa Misitu – Participatory Forests Management (PFM).
 
Vijiji hivyo vimeanza kunufaika na umilikishwaji huo. Kutokana na mavuno ya mbao, vijiji hivyo vimeweza kujipatia mamilioni ya fedha na kuzitumia kuboresha huduma zao za jamii, na hicho ndicho kinachowafanya wanakijiji wa Ruhatwe wajutie kosa walilolifanya la kutochangamkia ‘ofa’ ya MCDI.
 
Majuto hayo yanatokana na ukweli kwamba kilikuwa moja ya vijiji vya mwanzo kabisa kuendewa na kupewa ‘ofa’ hiyo ya kusaidiwa mchakato wa kutengewa misitu ya hifadhi, lakini hakukiichangamkia. Lakini baada ya kuona manufaa ya vijiji vya jirani vilivyokamilisha mchakato huo, kijiji cha Ruhatwe kilizinduka na kuanza mapambano yaliyodumu kwa miaka minane sasa ya kuwania kurejeshewa na kutengewa rasmi misitu wanayoamini ni yao ambayo kwa sasa ipo chini ya usimamizi wa kijiji jirani cha Migeregere.
 
Mapambano hayo yameibua mgogoro mkubwa wa mpaka kati ya kijiji hicho na kijiji cha Migeregere. Mgogoro huo una kila dalili kwamba usipomalizwa mapema utaingia kwenye umwagaji damu. Wakizungumza kwa jazba na ujumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) uliokitembelea kijiji hicho hivi karibuni, wanakijiji hao waliituhumu Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa pamoja na MCDI kwamba wanalalia upande wa kijiji cha Migeregere katika mgogoro huo.
 
“Sisi ni watu wenye damu poa; maana kama si hivyo tungeshajibu mapigo na damu ingeshamwagika. Hawa (kijiji cha Migeregere) si tu kwamba wamevamia misitu yetu miwili, lakini hata huu wa tatu ambao tumeanza mchakato wa kutaka tumilikishwe tayari nao wameuvamia, wanadai ni wao”, anasema Saidi Ali Ngauna ambaye ni mjumbe wa halmashauri ya kijiji hicho.
 
“Mgogoro kati ya kijiji chetu na kijiji cha Migeregere ni wa muda mrefu. Mara kadhaa wamekuja viongozi wa wilaya kujaribu kusuluhisha, lakini mpaka sasa hakuna mafanikio; japo walikuja na ramani zinazothibitisha kuwa eneo linalogombewa ni letu,” anasema Mwenyekiti wa kijiji hicho, Juma A. Juma.
 
Kijiji cha Ruhatwe kina wakazi 1,500 na kaya 250. Eneo la kwanza wanaloligombea lina ukubwa wa hekta 2,000, na la pili lina ukubwa wa hekta 1,120.
 
Kinachowatia uchungu wanakijiji wa Ruhatwe ni kwamba wakati mgogoro wa kuwania maeneo hayo ukiendelea, wenzao wa Migeregere wanaendelea kuvuna mipingo katika misitu ya maeneo husika, na hivyo kujipatia fedha ambayo huwasaidia kuboresha huduma zao za jamii; ilhali wao wameendelea kuwa na huduma zile zile duni za jamii.
 
Katika mkutano huo na JET, karibu kila mwanakijiji aliyepata fursa ya kuzungumza alielekeza kombora lake kwa ofisa wa MCDI tuliyeandamana naye kwamba asasi yake inakipendelea kijiji cha Migeregere katika mgogoro huo.
 
*Katika hali hiyo, ingawa JET ndio tuliokuwa wageni rasmi wa kijiji hicho, ilionekana dhahiri kwamba mkutano ule umegeuka kuwa wa malumbano kati ya wanakijiji dhidi ya ofisa huyo wa MCDI tuliyeandamana naye.
 
Hata baada ya ofisa huyo wa asasi hiyo ya Kilwa kuwahakikishia wanakijiji wale kwamba tatizo lililoibua mgogoro huo limekwisha, na kwamba wao (MCDI) wataanza hivi karibuni kushirikiana na kijiji hicho kuwasaidia kukamilisha mchakato wa kutengewa rasmi misitu hiyo, bado wana Ruhatwe hawakumwamini.
 
“Pamoja na kauli yako hiyo kwamba mgogoro umekwisha, naomba wanakijiji wenzangu tusipige makofi kushangilia mpaka hapo tutakapothibitisha kuwa kweli mgogoro umekwisha,” alitahadharisha mjumbe mmoja wa Kamati ya Maliasili ya kijiji hicho.
 
Mjumbe huyo wa Kamati ya Maliasili alisema ya kuwa, mgogoro huo hauwezi kwisha kwa sababu tu ya ofisa wa MCDI kutamka hivyo; bali utakwisha pale vijiji vyote viwili vitakapokutanishwa na vyote kuridhia kwamba kweli mgogoro umekwisha.
 
Akizungumza na ujumbe huo wa JET, mjini Kilwa Masoko, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Adoh Mapunda, alikiri kuwapo mgogoro wa mpaka kati ya vijiji hivyo, na kusema kwamba mgogoro huo si pekee katika wilaya hiyo. “Awali kabla wanavijiji hawajajua faida za kumilikishwa misitu, kulikuwa hakuna migogoro ya mipaka, lakini sasa migogoro imeibuka ya kugombea mipaka baina ya vijiji kwa sababu wamejua faida za misitu ndani ya maeneo yao,” alisema Adoh.
 
“Wilaya ya Kilwa ni kubwa mno. Ina ukubwa wa kilomita za mraba 13,000. Ina misitu mingi. Awali kabla wanavijiji hawajajua faida ya misitu, waliokuwa wakinufaikanayo ni Wachina waliokuwa wakifanya biashara haramu ya magogo, lakini sasa wanavijiji wameamka, na wameanza kuichangamkia misitu baada ya kuona faida yake,” anasema Mapunda.
 
Kwa mujibu wa maelezo yake, utambuzi huo chanya wa wanavijiji ndio ambao umeibua migogoro ya mipaka baina ya vijiji – migogoro ambayo Halmashauri yake imekuwa ikiitatua na kuimaliza, na sasa imebakia mitatu tu ukiwamo huo kati ya kijiji cha Ruhatwe na Migeregere. “Changamoto tuliyonayo ni kushughulikia migogoro hii inayoibuka ya vijiji kugombea mipaka. Mpaka sasa migogoro iliyobakia wilayani ni mitatu tu.
 
Tumepanga ndani ya miezi miwil hii iliyobakia ya mwaka huu tuimalize yote”, alisema Mkurugenzi huyo. Katika mazungumzo hayo na JET, Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Kilwa alithibitisha kile kilichoelezwa awali na wanakijiji wa Ruhatwe kwamba ramani za mipaka zilizopo zinaonyesha kuwa kijiji hicho ndicho mmiliki halali wa maeneo ilipo misitu hiyo na si kijiji cha Migeregere.
 
“Tumepania kumaliza mgogoro huo kabla mwaka huu haujamalizika,” alisema Mapunda ambaye siku mbili kabla yeye na ujumbe wake walisafiri kwenda kusuluhisha mgogoro mwingine wa mpaka kati ya kijiji cha Nanjilinji A na kijiji cha Miyui.
 
Naye Mtendaji Mkuu wa MCDI, Jasper Makalla, akizungumzia suala hilo la kuibuka migogoro ya mipaka baada ya vijiji kutambua faida za misitu, alisema kwamba migogoro hiyo hutatuliwa kwa njia shirikishi kwa kuwakutanisha pamoja wadau wote.
 
Makalla, ambaye NGO yake hiyo ndiyo inayovisaidia vijiji katika michakato ya kutengewa misitu ya hifadhi, na pia kuvisaidia namna ya kuiendeleza na namna ya kuivuna kiuendelevu, alisema kuwa, pia kuna migogoro mingine ambayo chanzo chake ni fedha zinazotokana na mavuno ya misitu.
 
“Ukiacha migogoro ya kugombea mipaka kati ya kijiji na kijiji, pia huibuka migogoro ya uongozi ndani ya kijiji chenyewe. Pesa zinazotokana na misitu zikishaanza kuingia ndipo migogoro ya uongozi ndani ya vijiji huibuka,” alisema Makalla.
 
“Tunatumia uwezo wetu kutuliza na kumaliza migogoro hii ya uongozi ndani ya vijiji kwa njia shirikishi, na siku zote tunawapigia kelele viongozi wa vijiji kuhusu umuhimu wa kuwepo uwazi (transparency) katika kusimamia na kuvuna misitu,” alisema Makalla.
 
Lakini si hivyo tu; kwani NGO hiyo pia huvisaidia vijiji kupata uzoefu wa namna ya kutunza kumbukumbu za mikutano muhimu ya kijiji, na pia kutunza hesabu za mapato na matumizi ya kijiji.
Mambo hayo mawili, kwa mtazamo wake, ndiyo chanzo kikubwa cha migogoro ya uongozi katika vijiji ambavyo vimeshaanza kunufaika na misitu ya hifadhi iliyotengewa rasmi na Serikali. Aidha, MCDI huvifundisha vijiji hivyo menejimenti ya fedha na masuala ya utawala, na pia hukagua mara kwa mara hesabu za vijiji hivyo na kuvipa maelekezo.
 
Hata hivyo, Makalla anasisitiza kwamba migogoro ya kugombea mipaka kati ya kijiji na kijiji bado inabakia kuwa ndio changamoto yao kubwa hasa wakati wa kutenga misitu ya hifadhi. “Chanzo kikubwa cha migogoro hii ni vijiji kuoneana wivu baada ya kuona wenzao wamenufaika zaidi na misitu yao.
 
Kwa kweli tunalazimika kuacha shughuli zetu nyingi kushughulikia migogoro hii, na hii maana yake ni kwamba tunalazimika pia kuelekeza fedha mahali ambako hatukupanga awali kuelekeza,” alisema Makalla.
 
Kwa kuzingatia kwamba wilaya ya Kilwa ina utajiri mkubwa wa misitu ambapo mgawanyo uko hivi: Msitu wa Serikali hekta 219,000, msitu wa hifadhi za vijiji hekta 185,000 na msitu wa Halmashauri hekta 54,000, ni dhahiri kwamba migogoro ya kugombea mipaka (misitu) itaendelea kusikika wilayani Kilwa.
 
Hata hivyo, jambo la kutia moyo ni kwamba kuibuka kwa migogoro hiyo ni ushahidi kwamba vijiji vya wilaya ya Kilwa sasa vinatambua manufaa ya kumiliki misitu, kuitunza na kuivuna kiendelevu, na ndiyo sababu vimeanza kuichangamkia kwa kasi.
 
Kulikuwa na hoja katika ujumbe huo wa JET kwamba pengine baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo visingeshawishika kuuza ardhi yao kwa mwekezaji wa kigeni kama vingekuwa vimefikia kiwango kilichofikiwa hivi sasa cha uelewa wa manufaa yatokanayo na misitu kama ikilindwa, kuendelezwa na kuvunwa kiendelevu.
 
Hoja hiyo inatokana na hisia za majuto ya baadhi ya wanakijiji wa Nainokwe kwamba wasingetoa ardhi kubwa kiasi kile kwa mwekezaji anayeitwa Bioshape, na kwa bei ile ndogo kama wangelijua kwamba wangenufaika na misitu hiyo kama wanavyonufaika hivi sasa.
 
Miaka minne iliyopita, kampuni ya Bioshape ilinunua maelfu ya hekta za ardhi katika vijiji vya wilaya hiyo, zikiwamo hekta 16,890 za kijiji cha Nainokwe, kwa ajili ya kilimo cha mibono.
 
Hata hivyo, mpaka sasa kampuni hiyo haijaiendeleza ardhi hiyo, na habari za kuaminika ni kwamba imetelekeza maeneo hayo baada ya kumaliza kuvuna Mipingo, na kwamba hisia za wanavijiji wengi ni kuwa lengo kuu lililokuwa limejificha la kampuni hiyo lilikuwa ni kuvuna Mipingo na kuisafirisha nje ya nchi, na si kulima mibono!
 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa MCDI, Jasper Makalla, aliwaambia waandishi hao wa JET kwamba asasi yake haikushirikishwa katika mchakato wa vijiji kuuza ardhi kwa Bioshape. “Mchakato ulikuwa wa siri na mkataba ulikuwa ovyo. Tungekuwa tumeshirikishwa tungevishawishi vijiji visiukubali mkataba ule,” alisema Makalla. Akizungumzia suala la kampuni hiyo ya Bioshape, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Adoh Mapunda, alithibitisha kwamba hakuna mibono iliyopandwa mpaka sasa, na kwamba kampuni hiyo imetelekeza eneo la mradi.
 
“Suala hili ni nyeti kwa kuwa linahusu masuala ya kisheria. Kimsingi, maelfu ya hekta hizo bado ni mali ya kampuni hiyo ingawa imetelekeza ardhi hiyo. Suala hili liko ngazi za juu na linashughulikiwa kutafuta ufumbuzi,” alisema mkurugenzi huyo.
 
Vyovyote vile, baada ya vijiji vya wilaya ya Kilwa kutambua manufaa vinayoweza kupata vitengewapo rasmi misitu ya hifadhi, na hasa vinapoilinda na kuivuna kiendelevu, hakuna tena kijiji kinachozungumzia suala la kuuza ardhi kwa wawekezaji wa kigeni.