Wanavijiji Kilwa waanza Kukatiwa bima za afya

MIAKA mitatu iliyopita Mzee Henjewele Juakali (78) alikuwa akiishi kwa hofu kubwa kutokana na afya yake kuzorota kwa sababu ya uzee. Asili ya hofu hiyo ni kipato chake kuwa kidogo kiasi cha kushindwa kugharimia gharama za matibabu kila auguapo.
 
*Hivi sasa Mzee Juakali haishi tena na hofu hiyo – shukurani kwa msitu wa hekta 8,000 unaoitwa Kijawa ambao kijiji chake cha Nainokwe umetengewa na Serikali chini ya mpango wa Menejimenti (ulinzi) Shirikishi ya Misitu – Participatory Forests Management (PFM).
 
Mzee Juakali ni mmoja wa wazee 22 wa kijiji hicho kilichopo kilomita 93 kutoka Kilwa mjini, ambao wamewekewa bima ya afya na serikali ya kijiji kwa pesa zinazotokana na mavuno ya msitu huo.
 
Lakini mafanikio ya kijiji hicho yanayotokana na msitu huo wa hifadhi waliotengewa hayaishii tu katika kuwawekea bima wazee. Kutokana na mapato hayo kijiji hicho pia kimeweza kujenga nyumba ya mtendaji wa kijiji na hata kutoa huduma ya chakula katika shule yao ya msingi.
 
Wakizungumza na ujumbe wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) uliokitembelea kijiji hicho hivi karibuni, wakazi wa kijiji hicho wanakiri kwa furaha kwamba mpango huo wa PFM umeyabadilisha mazingira yao.
 
“Tunaishukuru Serikali, tunalishukuru Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo la Kilwa (MCDF); na tunawashukuru wahisani wote kwa kutusaidia kubadilisha maisha yetu”, alisema Kaimu Mwenyekiti wa kijiji hicho, Yasin Abdallah.
 
Serikali imekuwa ikishirikiana na NGOs kadhaa, ikiwamo hiyo ya Mpingo kuendesha mradi wa Mama Misitu katika wilaya hiyo unaofadhiliwa na nchi za Norway na Finland. Mradi huo umeleta mwamko mkubwa katika vijiji vya wilaya hiyo katika suala zima la kutengewa misitu ya hifadhi, kuitunza na kuivuna kiendelevu.
 
Kwa mujibu wa Kaimu Mwenyekiti huyo wa kijiji, msimu wa mwaka jana (2011/2012) Serikali ya kijiji ilijipatia Sh milioni 13 kutokana na mavuno ya msitu huo na ziligawanywa kwa utaratibu ufuatao: Serikali ya kijiji (asilimia 50), Kamati ya Kijiji ya Maliasili (asilimia 45) na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (asilimia 5).
 
“Fedha zinazotengwa kwa ajili ya kamati ya kijiji ya maliasili ni kwa ajili ya kugharimia doria ndani ya msitu, vifaa n.k wakati ambapo fedha zinazotengwa kwa ajili ya serikali ya kijiji ni kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii ikiwa ni pamoja na shughuli nyingine kama hiyo ya kuwakatia wazee bima za afya,” alisema.
Lakini simulizi ya mafanikio inayosisimua kushinda zote kwenye orodha ya vijiji vya wilaya ya Kilwa vilivyotengewa misitu ya hifadhi, ni ile ya kijiji cha Nanjilinji “A”.
 
Kijiji hicho kimeweza kujiingizia Sh milioni 32.5 kutokana na mavuno ya msitu katika kipindi cha miezi miwili tu. Aidha, kati ya sasa na Desemba 2012, kijiji kinatarajia kujiingizia Sh milioni 100.
 
“Kwa kweli mafanikio ya kijiji hiki yanasisimua,” Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo la Mpingo, Jasper Makalla, aliuambia ujumbe huo wa JET na kuongeza: “Wana msitu mdogo wa hekta 61,000 lakini bado wameweza kupata mafanikio makubwa kushinda vijiji vingine ambavyo vina misitu mikubwa zaidi”.
 
Kutokana na mapato hayo, kijiji hicho kimeweza kutumia Sh milioni 15 kununua pikipiki kwa ajili ya kuimarisha doria ndani ya msitu wao.
 
Fedha nyingine zilielekezwa kwenye kuboresha huduma za maji na afya, na pia kununua vifaa vya kuvunia kama vile misumeno, kofia ngumu n.k, na pia vifaa vya ulinzi wakati wa doria.
 
“Kijiji hiki cha Nanjilinji “A” kina ndoto kubwa ya kujenga shule yake ya msingi kutokana na mavuno ya msitu kwa sababu kwa sasa shule iko katika kijiji cha Nanjilinji “B” ambako ni mbali kidogo,” alisema Makalla.
 
Kwa makadirio ya Bwana Makalla, kijiji cha Nanjilinji “A” kinaweza kujiingizia mapato ya Sh milioni 297 katika kipindi cha miaka mitano kutokana na mauzo ya magogo ya Mpingo tu. Katika kipindi hicho kijiji kinatarajiwa pia kujiingizia Sh milioni 288 kutokana na mauzo ya mbao za mti wa Msenjele, Sh milioni 122 kwa Mkongo, Sh milioni 325 kwa Mninga Jangwa, Sh milioni 137 kwa Mninga Bonde na Sh milioni 121 kwa Msufi Pori.
 
“Kwa mchanganuo huo, kama kijiji hicho kitapata wateja wazuri kwa miti yote hiyo, mapato yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni zaidi ya shilingi bilioni moja,” anasema Ofisa Mtendaji Mkuu huyo wa asasi ya Mpingo Conservation and Development Initiative (MCDI) ya Kilwa.
 
Makalla aliuambia ujumbe huo wa JET kwamba asasi yake ya MCDI imefarijishwa na mafanikio ya kijiji hicho, na hasa ikizingatiwa kwamba ndio iliyokitafutia kijiji hicho mteja mzuri wa mbao au magogo ya mti wa Mpingo.
 
“Sisi ndio tuliowatafutia mteja huyo wa Arusha ambaye ni kampuni inayoitwa Sound and Fair Company.
 
Kwa bei ya Serikali, mita moja ya ujazo ya Mpingo ni Sh 180,000 lakini mteja huyo amekuwa akinunua meta hiyo moja kwa Sh 250,000”, alisema Makalla. MCDI ilianza kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuvisaidia vijiji vya wilaya hiyo kukamilisha mchakato wa kutengewa misitu ya hifadhi mwaka 2004.
 
“Tulianza mwaka 2004 na vijiji viwili, lakini sasa idadi ya vijiji imefikia 10,” alisema Makalla.
 
Kwa mujibu wa Makalla, MCDI si tu kwamba inavisaidia vijiji hivyo kukamilisha mchakato wa kutengewa rasmi misitu ya hifadhi na serikali, lakini pia huvisaidia namna ya kuitunza na kuivuna kiendelevu. Pia huwafundisha viongozi wa vijiji hivyo namna ya kutunza vitabu vya mapato na matumizi, masuala ya pesa na utawala na namna ya kushirikisha wanavijiji wote katika masuala yanayohusu utunzaji wa misitu yao na mapato na matumizi.
“Si tu kwamba tunawasaidia kukagua vitabu vyao vya hesabu ili kuhakikisha mambo yako sawa, lakini pia uhudhuria mikutano yao ya vijiji ili kujithibitishia kwamba kila kitu kinachohusu misitu yao kinawekwa wazi mikutanoni,” alisema Makalla.
 
Kwa mujibu wa maelezo yake, kati ya vijiji hivyo 10, tayari vijiji vitano vimeshaanza kupata mafanikio kutokana na mavuno endelevu ya misitu waliyotengewa chini ya mpango huo wa Serikali wa Ulinzi Shirikishi wa Misitu.
 
Ni kwa sababu ya mafanikio yaliyokwisha kuonekana mpaka sasa, vijiji vingine vya wilaya hiyo navyo vinataka kutengewa rasmi misitu yao.
 
Chini ya mgawanyo wa misitu ya wilaya ya Kilwa, hekta 219,000 ni za msitu wa Serikali, hekta 185,000 ni kwa ajili ya misitu ya hifadhi ya vijiji na hekta 54,000 ni msitu wa Halmashauri ya Wilaya.
 
Ni kwa sababu pia ya kutambua mafanikio vinayoyapata kutokana na misitu hiyo, vijiji hivyo havina huruma na watu wanaoharibu misitu yao kwa kuchoma moto au wanaoshiriki biashara za magendo ya mazao ya misitu.
 
Ndiyo sababu karibu katika vijiji vyote ambavyo JET ilivitembelea wakati wa ziara hiyo, suala la doria linapewa kipaumbele.
 
Wakati ambapo kijiji cha Nanjilinji “A” kimefikia hatua hata ya kununua pikipiki kadhaa kwa ajili ya doria, vijiji vingine vimetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa baiskeli kadhaa.
 
“Suala la doria katika kijiji chetu cha Kikolle si la mzaha hata kidogo. Linapokuja suala la doria, hakuna cha mwanamke au mwanamume – wote tunashiriki,” alisema Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mwinyimkuu Hamad Hawadh.
 
Ushiriki wa wanawake katika doria kwenye misitu ya kijiji ulithibitishwa na mmojawao. “Najua sote tunanufaika na misitu hii, na ndio maana sioni tatizo kushiriki doria, na hata waume zetu wanalijua hilo na wameridhia,” Mama Mwanaisha Likoko wa kijiji hicho cha Kikolle aliuambia ujumbe huo wa JET.
 
Lakini ushiriki wa wanawake hauishii tu katika suala la doria ndani ya misitu ambayo vijiji vimetengewa; bali pia huonekana katika safu za uongozi. Karibu vijiji vyote ambavyo JET ilivitembelea wakati wa ziara hiyo, kikiwamo hicho cha Kikolle, idadi ya wanawake katika kamati muhimu ya kijiji ya maliasili ni kubwa.
 
Kijiji hicho cha Kikolle kimeweza pia kujenga nyumba ya mtumishi wa zahanati ya kijiji (Mama Mkunga) na pia kisima cha maji. “Awali huduma hizi tulikuwa tukizipata kupitia Halmashauri, lakini sasa tunazitoa huduma hizo sisi wenyewe kutokana na pesa za mavuno ya msitu wetu,” alisema Hawadh.
 
Kijiji hicho kina msitu wenye ukubwa wa hekta 459 wenye miti aina ya Mpingo, Mninga, Mkuruti na Mtondoo. Jambo jingine la kutia moyo ni kwamba karibu katika vijiji vyote hivyo, kuna sheria ndogo ndogo ambazo wanavijiji wameziweka kwa ajili ya kulinda msitu wao. Kwa mfano, katika kijiji cha Nainokwe, mwanakijiji anayekamatwa akichoma msitu hutozwa faini ya Sh 50,000.
 
Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa ambayo wilaya ya Kilwa imeyapata katika utekelezaji wa mpango huo wa Serikali wa Ulinzi Shirikishi wa Misitu (PFM), zipo changamoto au matatizo kadhaa kama vile kuibuka kwa migogoro ya mipaka kati ya vijiji na uchomaji moto misitu.
 
Hayo ni matatizo au changamoto ambazo Halmashauri, kwa kushirikiana na MCDI na wanavijiji, inajitahidi kuyatatua; lakini ni dhahiri yapo mengine ambayo ni makubwa na ya hatari zaidi.
 
*Moja kati ya hayo ni uvamizi wa mifugo mingi katika misitu ya wilaya hiyo inayotokea wilaya za Mbarali (Ihefu) na Igunga (Tabora). Si siri kwamba mifugo ya wafugaji hawa wanaohamahama imeharibu misitu mingi kote ilikopita.
 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, Adoh Mapunda, anakiri kuwepo kwa tatizo hilo kwa kueleza kwamba zaidi ya ng’ombe 13,000 wameingizwa wilayani kwake kutoka Ihefu na Igunga.
 
“Idadi hiyo ni kubwa mno kwa wilaya yetu, na hivyo tumechukua hatua ya kupiga marufuku wafugaji wengine kuingiza mifugo wilayani mwetu. Wapeleke kwingine,” anasema mkurugenzi huyo.
 
*Lakini tatizo jingine ambalo kwa sasa halionekani, lakini ni la hatari zaidi ni kwamba upandaji miti mipya ndani ya misitu hiyo ya hifadhi ni mdogo mno, na ile inayoota yenyewe kwa njia ya asili ni michache mno.
 
Karibu miti yote yenye bei nzuri katika misitu yote ambayo ujumbe huo wa JET uliitembelea katika ziara hiyo imesheheni miti mikubwa na ya umri mkubwa (miaka 100 na zaidi) na iliyopandwa enzi za mababu.
 
Si siri kwamba kwa kasi hii ya sasa ya uvunaji misitu, muda si mrefu maeneo mengi yatakosa miti mingi mikubwa yenye umri wa kuvunwa; maana ile iliyopandwa au kuota enzi za mababu itakuwa imekwisha.
 
Kwa hakika, wilaya ya Kilwa ndiyo wilaya pekee nchini ambayo bado katika misitu yake unaweza kuona miti aina ya Mpingo.
 
Kwingineko nchini miti hiyo imeshavunwa yote na kutoweka misituni, na hakuna juhudi zozote za kupanda mipya; achilia mbali ile inayoota yenyewe kwa njia ya asili.
Pengine hii ndiyo changamoto au tatizo kubwa ambalo wanavijiji, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na NGOs kama MCDI, wanapaswa kuelekeza nguvu zao kulikabili; vinginevyo neema ya sasa ya mapesa yanayotokana na mavuno ya Mipingo inaweza kuwa ni ya miaka michache tu.
 
Lakini tatizo jingine kubwa linalokabili baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo ni kule kuitegemea mno MCDI kwa kila kitu. Katika kijiji kimoja ambacho JET ilikitembelea, wajumbe wa Halmashauri ya kijiji walioombwa wakutane na wageni hao wa JET walitarajia mwishoni kupewa bahasha zenye posho zao za kikao kutoka MCDC!
 
Bahati mbaya kwao, ofisa wa asasi hiyo aliyeandamana na ujumbe huo wa JET hakuwa na posho hizo za wanakijiji kwa sababu hakuona mantiki ya kuwalipa wajumbe hao kwa kushiriki kikao cha aina hiyo cha muda mfupi tu.
 
Ilikuwa ni dhahiri kwa JET kwamba suala la fedha linapewa kipaumbele kwa viongozi hao kuliko dhana ya kujitolea katika shughuli zinazohusu maendeleo yao wenyewe.
 
Mtazamo wa namna hiyo kwa wanavijiji ni wa hatari. Ni hatari kwa maana MDCI ni NGO, na kama zilivyo NGOs nyingi nchini, fedha hutoka kwa wafadhili wa kigeni. Je, vijiji hivyo vitakuwa katika hali gani siku wafadhili hao wa kigeni wakisitisha msaada kwa NGOs nchini?
 
Suala hili la vijiji hivyo kutegemea mno fedha za wafadhili katika kulinda na kuitunza misitu yao ya hifadhi lilithibitishwa na mtendaji mkuu wa MCDI, Bwana Makalla ambaye alisema kuwa vijiji vingi vitaathirika iwapo MCDI itaacha kuvisaidia.
 
“Kama MCDI tukiondoka, si tu baadhi ya vijiji hivyo vitayumba, lakini pia Halmashauri itayumba hata kama italipa kipaumbele cha juu suala hilo la utunzaji misitu. Na hiyo ni kwa sababu Halmashauri inakabiliwa na tatizo sugu la upungufu wa rasilimali watu na vitendea kazi,” alisema Makalla.
 
Wadau wote walioulizwa kuhusu suala hilo wakati wa ziara hiyo ya Kilwa walikubaliana katika jambo moja kubwa: Kwamba ili vijiji visitetereke wakati fedha za wahisani zitakapokoma, ni vyema vikayatumia vyema mapato vinayoyapata sasa kutokana na mavuno ya misitu kujijengea uwezo wa kujitegemea huko baadaye kwa asilimia 100.
 
Hii pengine ndiyo changamoto kubwa na nyeti kushinda nyingine zote kati ya vijiji vile 10 vya wilaya ya Kilwa ambavyo vimeshaanza kufaidi fedha za mavuno ya misitu chini ya mpango wa Serikali wa Menejimenti Shirikishi ya Misitu nchini.