Wazanzibari vinywa wazi wangoja hatma ya mafuta, gesi

Na Haji Nassor, Pemba
KWA miaka mingi sasa kumekuwa na minong’ono isiyokwisha kwamba Zanzibar ina hazina ya mafuta na gesi asilia. Hii ilianzia mbali tokea enzi za ukoloni na naendelea hadi leo; lakini hakuna anaefahamu ukweli kuhusu uwepo au kutokuwepo kwake.

Uchunguzi umegundua, tokea miaka ya 1920, serikali za Marekani na Uingereza, zilionesha hamu ya kufanya utafiti wa mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki na mataifa jirani kama Ethiopia. Hamu ya mataifa haya ilitokana na kuwepo ishara ya uvujaji wa mafuta (oil spill) katika baadhi ya sehemu kutoka ardhini. Uvujaji wa mafuta ulionekana katika nchi za Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanganyika na hatimae Zanzibar. Katika Zanzibar uvujaji wa mafuta uliifanya serikali ya kikoloni kuandaa mazingira ya kisheria ili kuendeleza utafiti ambapo kampuni za Shell na British Petroleum (BP) zilipewa vibali kufanya utafiti wa mafuta mwishoni mwa miaka ya 50. Utafiti ulifanywa kwa maeneo ya Unguja na Pemba isipokuwa maeneo nyeti kimazingira kama vile kisiwa cha Fungu Mbaraka. Kisiwa hiki kiliachwa kwa sababu ni makazi ya aina mbali mbali za ndege, hivyo utafiti ungeathiri maisha ya viumbe hawa.

MAENEO YA UTAFITI
Uchunguzi umegundua utafiti ulihusiha uchimbaji wa visima vifupi na virefu katika maeneo mbali mbali yaliyochaguliwa. Kwa mfano visima viwili virefu; kimoja Kama kisiwani Unguja na chengine Tundauwa Pemba, vilichimbwa. Visima hivi vilitoa taarifa nzuri za uwezekano wa kuwepo mafuta na wataalamu walipata hamu ya kuendeleza shughuli za utafiti, hata hivyo hawakufanikiwa kupata mafuta katika visima hivyo. Hii inamaanisha, taarifa kutoka visima hivyo ilionesha kuwepo mazingira ya kiijiolojia ya uwezekano wa kuwepo mafuta na gesi asilia lakini kulihitaji utafiti zaidi kuthibitisha uwepo wa rasilimali hizo.

BAADA YA MAPINDUZI
Baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na baada ya Zanzibar kuungana na Tanganyika (1964) na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katiba ya Muungano iliipa serikali ya Muungano uwezo wa kusimamia shughuli zote za mafuta na gesi asilia. Shirika la maendeleo ya petroli (UPDC), ndilo lililopewa uwezo wa kufanya tafiti kwa maeneo yote ya Tanganyika na iliyokuwa Jamhuri ya Zanzibar kabla ya muungano. UPDC ndilo lililokuwa na mamlaka ya kugawa vitalu vya utafiti wa mafuta kwa Jamhuri yote ikiwemo maeneo ya Zanzibar kwa kuwa sasa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ilipofika miaka ya 1980, UPDC ikatoa vibali kwa kampuni kubwa za mafuta duniani kufanya tafiti kusini mwa Pemba, maeneo ya baharini magharibi ya kisiwa na mashariki mwa Unguja na Pemba kwa kutumia tafiti mtetemo (seismic exploration). Taarifa zilithibitisha uwepo wa mazingira ya mafuta, hata hivyo utafiti zaidi wa kisasa ungeweza kuthibitisha kuwepo rasilimali hiyo. Mnamo miaka ya 2000, shirika la TPDC liliingia mikataba ya vitalu kadhaa vya mafuta; miongoni ya vitalu hivyo ni vitalu nambari 9, 10, 11 na 12 mashariki ya visiwa vya Pemba na Unguja.

Vile vile Shirika na Wizara ya Nishati waliingia mkataba mwingine katika kitalu kilichopo kati ya Pemba na Tanga mahala ambapo kumbukumbu zinaonesha kumekuwa na dalili za wazi za kuwapo mafuta kutokana na kuonekana ishara ya uvujaji wa mafuta mara kwa mara. Vitalu 9, 10, 11 na 12 vilipewa kampuni ya Shell ya Uholanzi na kitalu cha kati ya Tanga na Pemba walipewa kampuni ya Antrim ya Canada ambayo baadaye waliuza sehemu ya kampuni yao kwa kampuni ya RAK Gas ya Ras Al Khaimah.

Hata hivyo, kwa kuwa vitalu hivi vipo katika eneo la Zanzibar kabla ya Muungano, serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikataa shughuli zozote kufanyika mpaka suala la mafuta na gesi liondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.

IDARA YA NISHATI NA MADINI-ZANZIBAR
Kwa sasa idara ndiyo yenye uwezo wa kusimamia masuala ya mafuta na madini Zanzibar kwa kuwa bado serikali ya Mapinduzi haijaanzisha shirika lake kusimamia rasilimali hizi. Mkurugenzi wa idara hii, Mohamed Abdalla Mohamed, anasema kawaida tafiti za mafuta ni ghali mno na ni kampuni kubwa tu ndio zenye uwezo wa kufanya hivyo. Hivyo, anasema serikali inaliendeleza suala hili kwa hadhari kubwa kwa kuandaa mazingira ya kisera, kisheria, kijamii na miundombinu kabla ya kualika kampuni kufanya utafiti.

“Serikali kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinashirikiana kwa karibu ikiwa ni pamoja kuandaa mabadiliko ya kisheria ili Zanzibar isimamie wenyewe utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia,” anasema. Kwa kuwa suala la mafuta linagusa kila sekta, anasema halipaswi kuchukuliwa maamuzi ya pumba vyenginevyo linaweza kusababisha athari kubwa baadae kiuchumi, kimajii na kimazingira.

Kwa mfano anasema, kabla ya shughuli za utafutaji, uchimbaji na hatimae uzalishaji kuanza, lazima idadi kamili ya Wazanzibari ijulikane kwa kuwa shughuli za mafuta zinawavutia wengi, wakiwemo wageni. “Hivi sasa tupo milioni 1.3 lakini inawezekana idadi ikaongezeka katika kipindi cha utafiti, uchimbaji na uzalishaji; kumbe wengi wa waliozidi watakuwa si Wazanzibari ingawa inawezekana wakawa na vitambulisho vinavyowatambulisha kwamba wao ni Wazanzibari, hivyo wakawa wanapatiwa huduma sawa na wenyeji,” anasema.

“Kwa kuwa wananchi wanatarajia mafuta yabadili maisha yao, kiafya, kiuchumi na kijamii, haitakuwa vizuri huduma za afya zinazopatikana sasa iwe sawa na zile zitakazopatikana baada ya mafuta kupatikana, hii ikitokea itasababisha wananchi kuhoji na hatimae inaweza kusababisha migogoro,” anasema. Hivyo, anasisitiza ni lazima serikali ihakikishe inazijengea uwezo taasisi zote zinazohusika na sekta ya mafuta ili pato litakalopatikana liweze kuwasaidia wananchi na uchumi wa taifa.

UWEPO WA MAFUTA
Bado ni mapema kuthibitisha uwepo wa mafuta Zanzibar, anasema Mkurugenzi huyo, ingawa anakiri kwamba tafiti zilizofanyika miaka ya 50 na 80 imethibitisha uwezekano wa Zanzibar kuwa na mafuta. Kwa mfano anasema vijiji vya Kama na Tundaua ambako visima virefu vilichimbwa, vimetoa matekoe mazuri ya kuwepo ishara ya kupatikana mafuta, lakini bado ni mapema kuthibitisha uwepo wa rasilimali hiyo hadi hapo tafiti utakapoanza kufanywa na kukamilika.

WATAALAMU WA MAFUTA
Mtaalamu wa masuala ya mafuta ambae hakutaka jina lake litajwe, anasema kuna kila dalili Zanzibar kuwa na mafuta, lakini tatizo ilikuwa nani awe mmiliki kati ya Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingawa suala hili sasa limeshapatiwa ufumbuzi.

“Suala Zanzibar kuwa na mafuta na gesi sio siri tena, limethibitishwa na kampuni mbali mbali za mafuta kuanzia miaka ya 50 na hadi leo kampuni hizo na nyengine zimeonesha nia ya kufanya utafiti,” anasema. Anasema kamwe kuwepo mafuta na gesi asilia pwani ya Afrika Mashariki hakuwezi kuvitenga visiwa vya Unguja na Pemba na hasa magharibi ya kisiwa cha Pemba kukosa rasilimali hizo. “Cha muhimu ni kufanya tafiti kama zilivyofanya nchi nyengine za Afrika Mashariki na kusini ambako kampuni za kigeni zimegundua gesi asilia nyingi na mafuta. Kwa mfano Msumbiji imegundua futi za ujazo trilioni 107 za gesi lakini baada ya kufanya utafiti wa kina,” anasema.

Katika masuala ya uchumi anasema kila kitu kina muda wake na masuala ya utafutaji mafuta ni masuala yanayoongozwa na msimu na kuendelea kuchelewa kufanya maamuzi juu ya suala hili kunalitia hasara taifa. Mtalaamu mwengine kutoka China, anasema Zanzibar ina uwezekano mkubwa wa kuwepo mafuta na gesi asilia na kuishauri serikali iharakishe utafiti na uchumbaji.

Akizungumza katika mafunzo ya mafuta na gesi katika chuo cha kimataifa cha biashara jijini Beijing kwa maofisa waandamizi wa serikali, anasema katika pwani ya Afrika Mashariki, Zanzibar inaongoza kuwa na rasilimali hiyo. "Zanzibar ni katika nchi yenye akiba kubwa ya mafuta na gesi asilia miongoni mwa nchi za mwambao wa pwani a Afrika Mashariki, itakuwa vizuri zaidi ikiwa seriakli itaanza matayarisho ya utafutaji na uchimbaji,”alisema.

Z’BAR NA MIKATABA YA MAFUTA
Kama sehemu ya juhudi za serikali kufanya utafiti wa mafuta, mapema mwaka 2014 serikali ilisaini mkataba na kampuni ya Ras Gas ya Ras Al-Khaimah kufanya utafiti wa awali (scaut) katika maeneo ya ardhi na baharini ili kupata uhakika wa uwepo wa rasilimali hiyo. Mkataba huu ulisainiwa katika kasri la Mfalme wa Rais AlKhaimah la Al-Dhait kati ya Katibu Mkuu wizara ya maji,ujenzi,nishati na ardhi ya Zanzibar, Ali Khalil Mirza na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Kamal Ahaya huku ukishuhudiwa na Mfalme, Sheikh Saud Bin Saqr AlQasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi. Aidha serikali ilisaini mkataba kama huo na kampuni ya Uholanzi ya Shell.

UFAHAMU WA WANANCHI KUHUSU MAFUTA, GESI
Elimu kuhusu mafuta na gesi asilia kwa wananchi bado iko chini sana kiasi ambacho wananchi wengi hasa wa vijijini, hawafamu faida na athari za rasilimali hii hata kama itapatikana Salim Haji Omar (45) mkazi mkazi wa Tundauwa, anasema ingawa kijiji chao kinatajwa kuwa na rasilimali ya mafuta, bado hawana ufahamu kuhusu rasilimali hiyo. Anasema hali hiyo inasababisha kutokuwa na ufahamu kuhusu rasilimali hiyo, faida na hasara zake na jinsi inavyoweza kusaidia kubadilisha maisha yao.

Ashura Mikidadi, mwenyeji wa kijiji cha Kama ambacho nacho kinatajwa kuwa na rasilimali hii, anakiri kuwa elimu ya mafuta na gesi bado haijawafikia wengi.Kwa maoni yake, anasema labda mamlaka husika zinasubiri utafiti ukamilike ndio shughuli ya kutoa elimu ianze.

WIZARA YA MAJI, NISHATI

Waziri wa wizara hii, Ramadhan Abdalla Shaaban, anasema wizara kupitia idara ya nishati na madini, iliandaa semina kutoa elimu  kuhusu mafuta na gesi asilia kwa wananchi, hata hivyo zilikuwa chache. Semina hizi mbili ziliwafundisha wananchi umuhimu wa mafuta na gesi asilia. “Mpaka sasa tumeandaa semina mbili kwa wananchi kuhusu masuala ya mafuta na gesi na kadiri hali itakavyoruhusu semina hizi zitatolewa ili wananchi wetu wawe na uelewa kuhusu rasilimali hii,” anasema.

MAANDALIZI YA SERIKALI

Waziri Shabaan, anasema katika kuhakikisha upatikanaji wa maafuta, serikali kupitia idara ya nishati na madini inaendelea kufuatilia shughuli za kusimamia upatikanaji wake, ikiwemo kushiriki vikao mbali mbali vya kitaifa na kimataifa kuhusu rasilimali hiyo. “Katika utekelezaji wa hili, idara imeshiriki mikutano mbali mbali iliyofanyika ndani na nje ya nchi; vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala ya nishati ya umeme (Nairobi, Entebe), mkutano mkuu wa mafuta na gesi wa Afrika Mashariki (EAPCE 2015) uliofanyika Kigali–Rwanda na mkutano wa kuitangaza Tanzania katika utekezaji wa masuala ya nishati, uliofanyika Den Hague–Uholanzi,” anasema. Pia serikali imeanza kufundisha wataalamu wake wa ndani masuala ya mafuta na gesi ili kuwa na utaalamu wa kusimamia rasilimali hizo.

SERA YA MAFUTA, GESI
Zanzibar tayari inaendelea na mchakato wa kuandaa sera yake ya mafuta na gesi; sera hii inagusa maeneo yote muhimu tokea utafutaji hadi uchimbaji. Pia imegusia masuala ya afya, usalama na mazingira (HSE), athari za mafuta na gesi katika matumizi ya ardhi, athari kwa sekta ya uvuvi,athari kwa sekta ya kilimo na misitu,athari kwa sekta ya utalii, athari kwa sekta ya maji safi, rasilimali ya baharini na masuala ya afya ya wafanyakazi, wananchi na maeneo mengine muhimu. Baada ya mchakato huu kukamilika, serikali itaandaa sheria ya mafuta na gesi pamoja na kuanzisha taasisi itakayosimamia rasilimali hii.

Mtaalamu wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Aboud Suleiman, anasema mchakato wa kutafuta mafuta unagusa sekta nyingi, ikiwemo afya, ardhi, maji, miundombinu, mazingira ya baharini na nchi kavu,uchumi na sekta nyengine muhimu, hivyo lazima serikali iwe na sera madhubuti itakayokabiliana na changamoto za biashara ya mafuta. Kwa mfano anasema, suala la mafuta linahusisha uchafuzi wa mazingira ya baharini hali ambayo kama haitadhibitiwa inaweza kuathiri mazalia ya samaki na uchafuzi wa fukwe ambazo ndio kivutio kikubwa cha watalii.

Kuhusu ardhi, anasema lazima kuwe na sera na sheria madhubuti ambazo zitaanisha malipo ya fidia ya ardhi za wananchi zitakazochukuliwa kwa shughuli za mafuta, ili kusiwe na malalamiko.

KIJIJI CHA TUNDAUWA
Kijiji hiki kiliopo magharibi mwa kisiwa cha Pemba katika wilaya ya Chake Chake ndicho kinachoangaliwa kwa karibu kuwa rasilimali hii. Nikiwa na shauku ya kujua ukweli, nalazimika kufunga safari hadi kijiji huko; lengo langu ni kupata maoni ya wanakijiji kuhusu rasilimali hii iliyobadili uchumi wa mataifa mengi duni. Kijiji hiki kimepakana na vijiji vya Chanjamjawiri, Shungi, Kiziwani, Kilindi na Papani kwa upande wa mashariki, Wesha na Tagoni kwa upande wa kaskazini na Mgelema na Wambaa kwa upande wa kusini.

Idadi ya wakazi wake ni kama 1,500, robo tatu wakiwa vijana, wanawake na watoto ambapo kilimo na uvuvi ndio uti wa mgongo wa uchumi wa kijiji. Shughuli za uvuvi na kilimo zinafanywa na wanawake na wanaume, ingawa wanaume ndio wakulima wakubwa zaidi.
Kiwango cha ufaulu wa wanafunzi si wa kuridhisha sana kutokana na watoto wengi kujiingiza katika shughuli za uvuvi, ingawa kijiji kina skuli yake. Huduma za kijamii kama maji safi na salama na huduma za afya zinapatikana kama ilivyo kwa vijiji vingi vya Pemba.

Hata hivyo, uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa mikoko umeshamiri katika kijiji hiki, hata hivyo juhudi zinazochukuliwa na wanakijiji kuzuia matumizi ya mikoko kwa shughuli za ujenzi na upigaji mkaa, kumesaidia kupunguza athari za kimazingira. Mzee Faki Haji Issa (82) baba watoto tisa na wajukuu 16 mwenyeji wa kijiji hiki, anasema tokea kijiji chao kitajwe kuwa sehemu yenye rasilimali ya mafuta, kimepata umaarufu.

“Nakumbuka wakati sisi wadogo walikuja wazungu wakazunguka kila kila pembe ya kijiji mpaka kwenye misitu na kuchimba mashimo,” anasema na kuongeza “baadhi ya alama zimepotea miaka ya hivi karaibuni.” Akizungumza kwa sauti ya chini kutoka na umri wake, anasema kuna kila dalili ya kijiji chao kuwa na rasilimali ya mafuta kwa sababu kisima kilichochimbwa miaka hiyo kimeonesha dalili ya mafuta.

“Ninachokwambia si cha uongo, unakiona kile kisima pale, ndicho kilichochimbwa na hao wazungu, kimejengwa na kinatuzwa kwa sababu tunaambiwa kina mafuta,” aliongeza. Baadae ananisindikiza katika eneo kilipo kisima; kumbukumbu zilizopo katika kisima hiki zinaonesha kilichimbwa miaka ya 1953 kikiwa na urefu wa futi 12,700. Kisima hiki kilichozibwa kwa mfuniko wa chuma na kufungwa kwa kufuli kinatumiwa kwa shughuli mbali mbali za utafiti.Bi Zainab Haji Kombo (83) licha ya kuwa hana ufahamu wowote kuhusu mafuta, anasema kijiji chao kimekuwa kikitembelewa na wageni wengi.

“Wewe si wa kwanza kuja hapa na wote wanaletwa kwangu kuniuliza kuhusu mafuta,” anasema na kuongeza “enzi hizo sisi wakubwa kidogo walikuja wazungu hapa wakachimba mashimo makubwa likiwemo lile pale (ananionesha) tukaambiwa wanatafuta mafuta.”
Fatma Yussuf (18) ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika skuli ya Tundaua, anasema amewahi kumsikia baba yake akisema kijiji chao kina rasilimali ya mafuta lakini pia anahadithiwa na baba yake kuhusu kisima kilichopo kijijini pao.

Fatma ambae ana matarajio makubwa kwamba siku moja kijiji chao kitabadilika, anasema kama rasilimali hiyo itapatikana maisha yao yatapiga hatua kubwa. Anasema matumaini ya kuwepo mafuta kijijini hapo ni makubwa mno hasa kwa vijana wa rika lake, ambao wengi wamejikuta wakiacha skuli na kutumbukia katika shughuli za uvuvi au kuozeshwa waume.
Khelefu Issa Kombo (42), anajishughulisha na uvuvi wa kienyeji kwa kutumia dau la urithi takribani miaka 14 sasa; kazi hii ndio inayomsaidia kutunza familia yake ya watoto watano, mke na mama yake. Anasema taarifa za kijiji chao kuwa na dalili za mafuta wamezipokea kwa matumaini makubwa kwa sababu anaamini yatabadili maisha yao.“Tunasubiri kwa hamu kubwa siku tutakayoambiwa kijiji chetu kina mafuta, huu utakuwa mwisho wa umaskini,” anasema Khelefu aliehitimu kidato cha nne skuli ya sekondari Shamiani.

MWISHO